SISI NI WAPITAJI DUNIANI


SISI NI WAPITAJI     DUNIANI
Shukrani kwa Mungu kwa nafasi hii ya kutafakari habari njema.
    Kama kichwa kinavyosema, wanadamu  wote ni wapitaji ulimwenguni. Hatujapewa makao ya milele hapa Duniani, lakini baada ya maisha ha ya kuna makao ya milele kwa kila mwanadamu. Mtume Paulo anasema katika waebrania 13:14, “ Maana hapa hatuna mji (makao) udumuo, bali twautafuta ule ujao”. Ni mji upi huo anasema wanautafuta  au wanatamani kuufikia. Ni mji au makao ya mbinguni, Ndivyo Yesu kristo alivyosema, “maana naenda kuwaandalia mahali (makao). Basi mimi  nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja (nitarudi) tena niwakaribishe kwangu ili nilipo mimi, nanyi mwepo” Yohana 14:2. Yesu aliwaeleza wanafunzi wake juu ya makao ambayo anakwenda kuwaandalia mbinguni.
                Biblia inaeleza wazi kuhusu maisha ya milele ya mwanadamu baada ya Dunia hii. Kuna makao ya aina mbili, Mbinguni- katika Ufalme wa Mungu na Yesu kristo, na Jehanamu mahali pa mateso na hukumu kwa wote waliomwasi Mungu, muumba wa Mbingu na nchi.
                BIBLIA, Neno la Mungu linasema, Mungu atamhukumu kila mwanadamu kulingana na matendo yake, wengine wataingia mbinguni – mahali pa raha, furaha na amani, wengine wataingia Jehanamu mahali penye mateso makali  na adhabu. Biblia inasema,  “nikawaona wafu wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa na kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni cha UZIMA, na hao wafu wakahukumiwa kwa kadri ya matendo yao. Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto (Jehanamu)” – Ufunuo 20:12,13,15.
                Hakuna mwanadamu anayetamani kukaa Jehanamu milele, hata hivyo Neno la Mungu linasema, yeyote ambaye jina lake halikuonekana katika kitabu cha UZIMA alitupwa katika ziwa la moto. Inatisha mno kutupwa katika ziwa  (bahari) la moto.Kitabu cha uzima kina majina ya watu wamwaminio Yesu na kuyatenda mapenzi ya Mungu. Je jina lako lipo katika kitabu cha Uzima?
                Biblia katika Mathayo25:35-46 inaeleza Jinsi mwana wa Adamu  (Yesu kristo) atakavyorudi mara ya pili ataketi katika kiti chake cha enzi, naye atawahukumu mataifa yote. Kila mwanadamu atasimama mbele zake (sisisote), naye atamhukumu kila mmoja kwa kadri ya matendo yake. Wale waliotenda mema wataingia katika uzima wa milele na waliotenda maovu wataingia katika adhabu ya milele. Ni jambo la kutisha kuwa siku moja tutasimama mbele za Mungu kuhukumiwa, Biblia inasema “ kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu  cha Mungu ……. na kila mtu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu” – Warumi 14:10,12.
                Kristo Yesu ndiye jibu pekee kwa maisha yetu wanadamu. Anasema, “mimi nalikuja ili wawe na uzima wawe nao tele” – Yohana 10:10. Yeye pekee ndiye anaweza kutufikisha mbinguni, anasema “mimi ndimi njia ya kweli na uzima. Mtu hawezi kufika kwa Baba (mbinguni)  pasipo mimi” – Yohana 14:6. Ni yeye pekee ndiye awezaye kumwokoa mwanadamu juu ya dhambi na hukumu ya mwisho.Yesu alikuja ili kila amwaminiye asipotee/asiangamie bali awe na uzima wa milele. Soma Yohana 3:16-19 Yesu hakuja duniani ili kuhukumu ulimwengu, bali wanadamu waokolewe kupitia kumwamini na kumfuata yeye – (Yohana 3:17)
                Biblia inasema, “amwamini yeye hahukumiwi, asiyemwamini (Yesu) amekwisha kuhukumiwa” – Yohana 3:18.Yeye amwaminiye
      Yesu anavuka kutoka mautini kwenda Uzimani.
                Ndugu yangu, ikiwa unamwamini Yesu, ninakutia moyo songa mbele katika kwa Jina la Yesu. Ikiwa haujampokea Yesu ,tambua kuwa pasipo yeye utahukumiwa kwenda Jehanamu. Mkubali yeye leo, tubu dhambi zako na uishi kwa ajili yake.
                Ili tuingie mbinguni ni lazima tuishi maisha matakatifu na safi mbele za Mungu. Pasipo utakatifu, hatutaingia mbinguni. “Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu“ –Mathayo 5:8. Pia Paulo anatuagiza, “ tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu ambao hapana mtu atakayomwona Mungu asipokuwa nao” – Waebrania 12:14 Ni hatari sana kwa mkristo kuishi maisha ya dhambi, kwa kuwa ataikosa mbingu.
                Mbinguni ni mahali pazuri, pa furaha kuliko mahali pengine popote. Tutamani kufika huko. Itazame mistari hii inayoeleza juu ya mbinguni, “ na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi,  mfano wa kioo” – Ufunuo 21.18; “ Na njia ya mji ule ni dhahabu safi kama kioo kiangavu”- Ufunuo 21:21.Pia ufunuo 21:2,4 inasema, Nami nikaona mji ule mtakatifu, wala mauti haitakuwepo, wala maombolezo ….” Oh mbinguni pana uzuri usioelezeka, hakuna njaa, magonjwa wala matatizo ya kiuchumi. Tuende sasa mbinguni, naam, kwa kutembea na Yesu tungali hai.
Jehanamu ni mahali pabaya mno. Ni mahali penye moto usiozimika, unaowatesa watu milele na milele. Neno la Mungu limeeleza juu ya Jehanamu kuwa ndani yake kuna kilio, maombolezo na kusaga meno. – (Mat 13:42, 13:50, 25:30), Ni hatari mno.
                Katika luka 16-18:-31, Yesu anaelezea maisha baada ya kufa ya tajiri mmoja na Lazaro maskini. Tajiri aliishi maisha ya anasa na maskini Lazaro alikuwa mcha Mungu. Baada ya kufariki kwao, Lazaro alichukuliwa hata mahali tulivu penye utele (mbinguni). Lakini Yule Tajiri aliingia katika mateso makali katika moto mkali. Mmoja alienda mbinguni na mwingine Jehanamu.
Hatima ya maisha ya mwanadamu ipo mikononi mwake. Ikiwa atamwamini na kumtii Yesu ataingia mbinguni, kinyume chake, hukumu ya kutisha mno, itakuwa mbele yake, yaani Jehanamu ya moto.
                Ndugu yangu, tusiipende dunia na anasa zake, tukiipenda dunia na uovu wake, ni dhahiri tutaikosa mbingu. Yesu alisema, “itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake”- marko 8:37. Itakufaidia nini mwanadamu kuupata ulimwengu na anasa zake, lakini
Ukaipoteza nafasi yako katika adhabu ya milele!!!!
      Yesu alikuja ili tuwe na uzima wa milele. Mungu anatupenda sana wanadamu, hata akamtuma Yesu. Yesu Kristo, mwana wa Mungu aliteseka msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Leo anatuita na kutukumbusha kuwa inatupasa kumpenda yeye na kumtii ili atufikishe mbinguni. Hapendi mtu yeyote apotee, bali awe na uzima wa milele.
Mungu akubariki kwa kusoma ujumbe huu. Hayakuwa mawazo ya kibinadamu, au ujuzi wa akili, bali niNeno la Mungu, llilo hai na kweli milele yote. Hivyo yaweke moyoni mwako, ukayatendee kazi.
Ikiwa haujampokea Yesu moyoni mwako  au ulirudi nyuma – ni muhimu kujikabidhi kwa Bwana YESU, kiri maneno haya ukiamini moyoni mwako.
Bwana Yesu, naja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Ninaomba unisamehe, nitakase kwa damu yako na uandike Jina langu katika kitabu cha Uzima. Ninakukaribisha moyoni mwangu uwe Bwana na mwokozi wangu tangu sasa na hata milele. Amen.
                Amini kuwa Yesu kristo ameingia ndani yako, shirikiana na wale wampendao ili uweze kukua ndani mwake.
Mungu wa Mbinguni akubariki.
Kwa mawasiliano zaidi;
0759 895181/0713049601
        Justo Mathew.

Comments

Popular posts from this blog

Mbinu za Shetani.